Baba wa familia akiwa pamoja na wanafamilia akionekana kutoa maelekezo kwa upole kiashiria cha malezi bora

Malezi
ni mchakato wa kumfundisha, kumwongoza na kumkuza mtoto ili akue akiwa na maadili, nidhamu, maarifa na stadi zinazomsaidia kuishi vyema katika jamii. Malezi bora yanajumuisha upendo, mawasiliano ya wazi, uangalizi wa karibu na mfano mzuri kutoka kwa mzazi au mlezi.

Mifano: 

-  Mtoto anapokushuhudia mzazi wake akiwaheshimu majirani, hata yeye hujifunza kuishi kwa heshima na mshikamano na watu wengine.

-  Mzazi unayemfundisha mtoto wako kupanga matumizi ya pesa ndogo ndogo unazompa, humsaidia kujua thamani ya fedha na namna ya kudhibiti tamaa.

Mambo 7 Anayopaswa Kufundishwa Mtoto kwa Ajili ya Kesho Yake

(i) Maadili na Heshima
Mtoto afundishwe kuishi na maadili mazuri kama kusema ukweli, kuepuka dhuluma na kuwaheshimu watu wa rika zote. Mfano: Mtoto anapomkaribisha mgeni nyumbani kwa heshima, hujenga tabia itakayomheshimisha hata akipata nafasi ya uongozi shuleni au kazini.

(ii) Nidhamu ya Muda
Mtoto aelezwe umuhimu wa kupanga na kutumia muda vyema kwenye masomo, michezo na mapumziko. Mfano: Mtoto anayejua kuamka mapema kwa ajili ya shule hutengeneza nidhamu ya kazi atakapokuwa mtu mzima.

(iii) Kujitegemea na Uwajibikaji
Afundishwe kufanya baadhi ya shughuli mwenyewe na kuwajibika kwa makosa yake. Mfano: Mtoto anapojifundisha kutandika kitanda chake kila asubuhi, anajijengea tabia ya kujitegemea na kutowategemea wengine kupita kiasi.

(iv) Thamani ya Elimu
Afundishwe kuitambua elimu kama nguzo ya maisha bora ya kesho. Mfano: Mzazi unapompeleka mtoto maktaba au kumsaidia kusoma vitabu, mtoto anapanda mbegu ya kupenda maarifa.

(v) Upendo na Huruma
Afundishwe kugawana, kusaidia na kushirikiana na wenzake. Mfano: Mtoto anayempa mwenzake penseli shuleni hujifunza roho ya mshikamano ambayo kesho inaweza kumsaidia hata katika kushirikiana kazini.

(vi) Ujasiri na Kujiamini
Mzazi umtie moyo mtoto kuzungumza na kushiriki shughuli bila woga. Mfano: Mtoto akipewa nafasi ya kuongoza dua au sherehe ndogo, anajijengea ujasiri wa kesho katika kukabiliana na changamoto kubwa.

(vii) Stadi za Maisha (Life Skills)
Mtoto apewe elimu ya kujua mambo ya msingi ya maisha kama kuitunza afya, kutumia pesa na mawasiliano bora. Mfano: Mtoto anayejifunza kupika chakula rahisi au kutunza usafi wa mwili, anakuwa na msingi wa maisha yenye afya na kujitegemea.

 Hitimisho

Malezi bora ni urithi mkubwa zaidi mzazi unaoweza kumwachia mtoto wako. Wazazi mnapoweka bidii kumfundisha mtoto maadili, nidhamu, ujasiri, elimu na stadi za maisha, wanamwandaa kuwa raia mwema na nguzo ya familia na taifa. Watoto wa leo ndio viongozi, walimu, madaktari, wajasiriamali na wabunge wa kesho. Tukiwalea vyema sasa, tunalijenga taifa lenye nguvu kazi yenye maadili na maarifa bora kwa vizazi vijavyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post